Luka 9:37–43
37 Kesho yake walipokuwa wakishuka kule mlimani, kundi kubwa la watu lilikutana na Yesu. 38 Hapo, mtu mmoja katika lile kundi akapaza sauti, akasema, “Mwalimu! Ninakusihi umwangalie mwanangu-mwanangu wa pekee! 39 Pepo huwa anamshambulia, na mara humfanya apige kelele; humtia kifafa, na povu likamtoka kinywani. Huendelea kumtesa sana, asimwache upesi. 40 Niliwaomba wanafunzi wako wamfukuze, lakini hawakuweza.” 41 Yesu akasema, “Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka! Nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini?” Kisha akamwambia huyo mtu, “Mlete mtoto wako hapa.” 42 Wakati mtoto huyo alipokuwa anamjia Yesu, yule pepo alimwangusha chini na kumtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu akamponya mtoto na kumkabidhi kwa baba yake. 43 Watu wote wakashangazwa na uwezo mkuu wa Mungu.
Habari hizi ni mfano wa nguvu na mamlaka ya Yesu juu ya vitu vyote vya kiroho na nguvu za giza. Vitu hivi kama mashetani, pepo, hata na Ibilisi, vyote ni viumbe ambavyo Mungu aliviumba. Viliumbwa naye vema ila wakawa waovu. Mungu ana mamlaka juu yao kabisa kwa kuwa ni viumbe vyake tu. Yesu anaonyesha mamlaka hiyo kwa kuwafukuza kwa kunena tu.
Yesu ana mamlaka juu ya nguvu zote za giza katika maisha yetu. Ni mwenye uwezo juu ya wachawi na roho chafu. Hata na wale waliofariki na wazimu si kitu mbele za Yesu.
Hasa Yesu aliwashinda nguvu hizi za giza wakati alipokufa msalabani. Yesu aliwashinda hapo kwa sababu Yesu alileta msamaha wa dhambi. Shetani hana mamlaka juu ya watu wamwaminio Yesu na hawezi tena kuwashtaki kwa kuwa wamehesabiwa haki kwa imani.
Wakolosai 2:13–15
13 Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu nyinyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa nyinyi uhai pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote; 14 alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani. 15 Huko Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake.
Katika Biblia kuna habari ya mchawi aliyejaribu kulaani watu wa Mungu lakini alishindwa kabisa kwa sababu Mungu aligeuza laana yake kuwa baraka (katika Biblia unaweza kusoma katika Hesabu 23).
Siku hizi watu wengi wanahofu laana au wanajitahidi kwa mila na desturi kujipatia baraka. Mara nyingi wanasisitiza matendo ya kufanya ili wapate kuepuka laana na kupata baraka.
Biblia inasema katika Yesu, kila mtu anayemwamini Yesu, Mungu amempa baraka zote za rohoni, na anatupa kwa neema yake. Si kwa kutenda au kutoa bali kwa upendo wake. Inaonyesha baraka kuu ni Roho Mtakatifu aliye Mungu mwenyewe kukaa ndani yetu na kutufanya upya kabisa, akiwa uhakika wa upendo wa Mungu kwetu na wokovu wa milele.
Wagalatia 3:13–14.
13 Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: “Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa.” 14 Jambo hili lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu alituahidia.