Mkristo ni mtu anayemwamini Yesu Kristo. Ni mtu aliyeacha miungu na dini nyingine ili ampokee Yesu kuwa Bwana na Mwokozi.
Kuwa mkristo sio jambo la ukoo wala kabila wala uraia. Mtu ye yote anaweza kumwamini Yesu Kristo na kuwa mkristo. Mtu wa kabila lo lote anaweza kuwa mkristo, kama wahadzabe, au waha, au wanyaturu. Tena, kuwa mkristo sio jambo la umri au jinsia. Mtu ye yote anaweza kumwamini Yesu Kristo, akiwa mtoto au babu, bibi au mtoto mchanga, mume au mke.
Tena, kuwa mkristo sio jambo la elimu, cheo, uwezo au kazi. Watu wadogo sana kama watumwa na watu wa umuhimu sana kama malkia wanamwamini Yesu Kristo na ni Wakristo. Mungu hana ubaguzi. Mkristo ni mtu ye yote ambaye anamwamini Yesu Kristo.
Yesu Kristo ni mtu aliyeishi miaka elfu mbili iliyopita. Alikaa katika taifa liitwalo Yudea, sehemu za mashariki kati. Yesu Kristo alifanya mambo ya ajabu, na alifundisha mambo mazuri juu ya Mungu na maisha. Watu wengi walimfahamu na kumpenda.
Matendo ya Mitume 10:37–38
Nyinyi mnajua jambo lililotukia katika nchi yote ya Wayahudi kuanzia Galilaya baada ya ule ubatizo aliohubiri Yohane. Mnamjua Yesu wa Nazareti na jinsi Mungu alivyomteua kwa kummiminia Roho Mtakatifu na nguvu. Mungu alikuwa pamoja naye; yeye alikwenda huko na huko akitenda mema na kuwaponya wote waliokuwa wamevamiwa na Ibilisi
Yesu ndiye Mfalme maalumu aliyetumwa na kutiwa mafuta na Mungu kuleta baraka na usalama. Ndiyo maana ya neno Kristo. Ni cheo chake Yesu, kama kusema Yesu Mfalme. Yesu ni mwokozi aliyetumwa na Mungu ili alete maisha bora, na aondoe shida ya uovu na kufanya upya ulimwengu mzima.
Yesu alionyesha kuwa ni mwenye uwezo wa kuponya wagonjwa na kutoa pepo. Hata na alituliza dhoruba na kuwalisha watu wengi kwa chakula kidogo. Lakini licha ya mema hayo, viongozi wa siku zile waliingiwa na hofu na wivu. Walishauriana na, wakijiunga na liwali aliye Mrumi, wakamwua Yesu kwa njia ya msalaba. Hii ndiyo njia ya warumi kuwaua wasaliti na wahalifu wabaya zaidi. Ni aina ya kifo iliyo ya aibu na maumivu sana, hata na wengi waliona aliyesulibwa kuwa amelaaniwa na Mungu.
Matendo ya Mitume 10:39–43
Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyotenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu. Walimuua kwa kumtundika msalabani; 40 lakini Mungu alimfufua siku ya tatu, akamfanya aonekane, 41 si kwa watu wote, ila kwa wale Mungu aliokwisha wachagua wawe mashahidi wake, yaani sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42 Alituamuru kuihubiri Habari Njema kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyeteuliwa na Mungu awe Mwamuzi wa walio hai na wafu. 43 Manabii wote waliongea juu yake kwamba kila mtu atakayemwamini atasamehewa dhambi zake zote kwa jina lake.”
Wakati Yesu alipokufa, watu wengi waliomwamini Yesu wakakata tamaa na kuhuzunika. Lakini siku ya tatu baada ya kufariki na kuwekwa kaburini, Yesu alifufuka. Akapata kuwa hai tena, lakini kwa uzima mpya usioharibika. Yesu akatokea kwa watu wengi, hata na akala nao kuthibitisha ni hai kweli na sio roho au mzimu. Kisha Yesu akapaa mbinguni ili atawale yote mbinguni na ulimwenguni, kama alivyosema.
Yesu Kristo awakaribisha watu waje kwake kwa wokovu, yaani, msamaha wa dhambi, uzima wa milele, na kupatana na Mungu. Anaweza kuahidi huo wokovu kwa sababu alifufuka na anaishi milele, na pia alitukuzwa kuwa mfalme wa mbingu na nchi.
Mathayo 11:28
Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
Yesu anawaita watu wa kila mahali kumpokea kama Bwana na Mwokozi. Mtu anaweza kumpokea Yesu kwa imani. Maana ya imani ni kumtegemea Yesu kwa wokovu, usalama na baraka na kujikabidhi kwake. Kumwamini Yesu ni kuamini alichoahidi juu ya kuleta wokovu, na kumtegemea alete wokovu huo huo.
Yohana 3:16
Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uhai wa milele.
Ikiwa mtu anamwamini Yesu, anasamehewa dhambi zake zote na uovu wake wa kusema, kutenda, na kufikiri. Anatakaswa na kuhesabiwa haki. Anapewa uzima wa milele. Amepatanishwa na Mungu na kufanywa mwana wake, akiwa na amani naye. Anaokolewa kabisa na Yesu. Si jambo mahali au ukoo anapotokea au jinsi alivyo. Kwa imani katika Yesu tunaokolewa.
Matendo ya Mitume 15:9, 11
Mungu hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani. … tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tutaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu.”
Mkristo ni mtu ye yote anayemwamini Yesu kuwa Mwokozi na kumtegemea Yesu atawala maisha yake kama Bwana. Anajitahidi kumtii Yesu na kumwishia kwa unyenyekevu na kutenda mema. Lakini, Mkristo ni mtu aliyesamehewa, sio mkamilifu. Mara nyingi Wakrito wanakosa na kufanya kinyume cha mapenzi ya Mungu. Bali kwa vile wanavyomwamini Yesu wako salama katika upendo wa Mungu maana Yesu alijitoa kwa dhambi zao zote.
Mkristo sio mtu aliyezaliwa katika familia ya kikristo, wala mtu atiiye sheria kikamilifu, wala kusali kanisani au kutoa sadaka. Mambo hayo yote ni mazuri, lakini hayamfanyi mtu kuwa Mkristo wala kumwokoa. Kama kumvalia tumbili kwa ngozi ya simba haimfanyi kuwa simba, pia na kufanya matendo ya kikristo haimfanyi mtu kuwa Mkristo. Kinachotakiwa ni imani. Imani yako ni katika nani?
Kila amwaminiye Yesu amesamehewa zote, amefanywa mwana wa Mungu, na atafufuliwa kwa uzima wa milele.
Yohana 3:36
Anayemwamini Mwana anao uhai wa milele; asiyemwamini Mwana hatakuwa na uhai wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake.
Kama unataka kujifunza zaidi katika ujumbe wa Biblia kuhusu wokovu, karibu kusoma kijikitabu hiki.